Friday, July 31, 2009

Dini zetu ni kikwazo.

Mola nakupa heshima,ulimwengu uliumba.
leo mimi natazama,wapo waloshayafumba.
Kisa wazi nakisema,mimi na wangu mchumba.
dini zetu ni kikwazo,e Mola tusaidie.


Sio siri nampenda,shairi nimeandika.
kwa mwingine sitoenda,mistari niliishuka.
vishawishi nitashinda,nilisema na hakika.
dini zetu ni kikwazo, e mola tusaidie.


Mapenzi hayana dini,kabila wala hayana.
semi hizi kulikoni,hatarini kuachana.
ya kweli yangu imani,kamwe siwezi ikana.
Mwenzangu yake imani,msimamo kesha weka.
dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Wazaziwe wamfunza,kiburi wamjazia.
dini yake kuitunza,msimamo wamwekea.
wazaziwe wanibeza,kifupi wanichukia.
dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Baba mama walionya,kupenda kuliniteka.
Tayari walishaona,uzoefu 'litumika.
yakwao sikuyaona,kupenda kulifunika.
Dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Mwanangu hebu tulia,wa diniyo tampata.
chunga kutokujutia,matatizo tayapata.
haya nayakumbukia,rafiki alinisuta.
dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Njia panda bado nipo,sina pa kuelekea.
Nipeni njia mkato,mapenzi nayajutia.
Hima popote ulipo,ushauriwo "tapokea.

Friday, July 24, 2009

Sio siri nakupenda.

Miaka ilishapita,magumu niliyavuka.
Visiki nilivipita,wa maisha kumsaka.
Nilijua 'tampata,papara sikuzitaka.
Sio siri nakupenda,kwa mwingine sitoenda.


Natamani uwe wangu,niambie nitulie.
Ilikuwa siri yangu,imebidi nikujuze.
Niwambie ndugu zangu,baraka watujalie.
Sio siri nakupenda, kwa mwingine sitoenda.


Usiku hata mchana,nakuwaza nisikie.
Mapenzi yalomapana,nipokee unifiche.
Sio leo wala jana,penzi langu litambue.
Sio siri nakupenda,kwa mwingine sitoenda.


Sina sababu kupenda, ulivyo waniridhisha.
Sitake mimi kukonda,wewe ndo yangu maisha.
Naapa sitokutenda,hima sitobabaisha.
sio siri nakupenda, kwa mwingine sitoenda.


Tamati nimeifika,nambie unachowaza.
Kwako nimefika,sijui kama wakwanza.
Wewe utachotamka,moyoni tanituliza.
Sio siri nakupenda, kwa mwingine sitoenda.

Thursday, July 16, 2009

YATIMA JAMA HURUMA.

Yatima waso hatia,huruma napowakuta.
mlo wajitafutia,si hakika kuupata.
jalalani kuchokona,chochote watachopata.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Magonjwa yawaandama,hakuna wa kuwatibu.
nani wa kuwatazama,maradhi yawaadhibu.
na chawa wawaandama,malazi yaso adabu.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Mikononi mwa polisi,mkong'oto kama kazi.
maisha ya wasiwasi,watumiwa kwenye wizi.
zawakosa na risasi, kifo kipo waziwazi.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Wengine pia hubakwa,ukimwi rahisi kupata.
Wengine hulawitiwa,makubwa na huwakuta.
miili yao yauzwa,
wengine kunufaika.
Yatima jama huruma, sio lao kusudio.


Wazazi nisikieni,tulieni msiruke,
ukimwi upo jamani,chunga usiwamalize.
malezi ni ya wazazi, walimwengu wako bize.
yatima jama huruma, sio lao kusudio.


Vijana siwasahau,kila jambo na wakati.
katu usijisahau,kuzaa kabla wakati.
wala usijejaribu,ngono siipe nafasi.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Yapo mengi yawasibu,siwezi yote eleza.
Sote na tunawajibu,kutoa tunachoweza.
Elimu kwao muhimu,hamasika kuwatunza.
Yatima jama huruma, sio lao kusudio.

Tuesday, July 14, 2009

NINI WAMETUFANYIA?

Uchaguzi mbili kumi,huo hapo wajongea.
Waja kuisaka kumi, wako waliolowea.
wametufanyia nini, jibu sharti kutupatia.
tuamke wajameni,tuchague wa kutusaidia.
Kura fika haki yako,umpendaye mchague.
hupotezi muda wako,uhakika wa badae.
nini wametufanyia,waulizwe bila woga.

Tarehe itawadia,kampeni kuzipiga.
Waongo utawajua,'tazijua zao soga.
uwezo kuzingatia, zawadi wakizimwaga.
nini wametufanyia,waulizwe bila woga.


Takrima usikubali,mzalendo 'ndo kigezo.
yule atayekujali, hela isiwe kigezo.
Usiukubali wali,wala tisheti za dezo.
nini wametufanyia,waulize bila woga.


Wageni watatujia,yakwao watatwambia.
nini watatufanyia,bayana kutuwekea.
zipi 'takuwa hatua,wasipotutimizia?
nini wametufanyia,waulizwe bila woga.

Kalamu naweka chini,jamani tuwe makini.
somo lipo akilini,mitano hiyo ni mingi.
nne moja fomesheni,kamchezo kasomeni.
nini wamefanya,waulizwe bila woga.