Friday, September 11, 2009

Jua ni la utosini.

Asubuhi kunakucha,na njia ninaishika,
Ninapokwenda naficha,'tasema ntakapofika,
Nitapata ya mchicha?,swali liso na hakika,
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Ni wangu tena ujio,fungua pesa upate,
Chanuo na mafagio,ina njoo nikupake,
Anjifu na mitandio,mikufu pia na pete,
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Huruma siku yapita, ndururu sijainusa,
Watoto mimi najuta,viumbe waso na kosa,
Mitaa ninaipita,wateja spati kabisa,
Jua linanifuata,katu halitaki susa,
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Machinga ndo kazi yangu,mtaa hadi mtaa,
Kazi yanipa machungu,ila sikati tamaa,
Nachoka haki ya Mungu,umande nilikimbia.
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Mlo bahati someni, mwenzenu nilichezea,
Chenga nyingi shuleni,vitabu sikushangaa,
wasomi mataikuni,tuso skuli twaduwaa.
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Siombee umachinga,miguu yote yauma,
Bora jela kutinga,jua la utosi noma,
Pesa haujaichanga,fasta jua lishazama.
Jua ni la utosini,linachoma si utani.

4 Comments:

Blogger Fadhy Mtanga said...

Ni jua la saa sita, lanichoma utosini,
Jasho langu sijafuta, bado nasaka juani,
H'ijashuka yangu nyota, initoe matesoni,
Ningali mimi naranda, na jua laniwakia.

Bado sijapata kitu, ndugu wamenikimbia,
Mi kwao si malikitu, natanga na yangu njia,
Hawajathubutu katu, mimi kunisaidia,
Ningali mimi naranda, na jua laniwakia.

September 11, 2009 at 12:21 PM  
Blogger Albert Kissima said...

Ni mvua au jua,jua nalifurahia,
mvua sio riziki,jua lanibariki,
mvua wapi 'ntapita,juani pesa ntapata.
Shukurani kaka Fadhy,mashairi kwako jadi.

September 12, 2009 at 4:48 AM  
Blogger Unknown said...

Hapa wamekutana wanamalenga...kaaazi kweli kweli

September 18, 2009 at 12:30 AM  
Blogger Albert Kissima said...

Shukrani kaka Shabani,karibu tena na tena mwanamalenga.

September 19, 2009 at 8:54 AM  

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home