Thursday, July 16, 2009

YATIMA JAMA HURUMA.

Yatima waso hatia,huruma napowakuta.
mlo wajitafutia,si hakika kuupata.
jalalani kuchokona,chochote watachopata.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Magonjwa yawaandama,hakuna wa kuwatibu.
nani wa kuwatazama,maradhi yawaadhibu.
na chawa wawaandama,malazi yaso adabu.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Mikononi mwa polisi,mkong'oto kama kazi.
maisha ya wasiwasi,watumiwa kwenye wizi.
zawakosa na risasi, kifo kipo waziwazi.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Wengine pia hubakwa,ukimwi rahisi kupata.
Wengine hulawitiwa,makubwa na huwakuta.
miili yao yauzwa,
wengine kunufaika.
Yatima jama huruma, sio lao kusudio.


Wazazi nisikieni,tulieni msiruke,
ukimwi upo jamani,chunga usiwamalize.
malezi ni ya wazazi, walimwengu wako bize.
yatima jama huruma, sio lao kusudio.


Vijana siwasahau,kila jambo na wakati.
katu usijisahau,kuzaa kabla wakati.
wala usijejaribu,ngono siipe nafasi.
yatima jama huruma,sio lao kusudio.


Yapo mengi yawasibu,siwezi yote eleza.
Sote na tunawajibu,kutoa tunachoweza.
Elimu kwao muhimu,hamasika kuwatunza.
Yatima jama huruma, sio lao kusudio.

3 Comments:

Blogger Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli kabisa inabidi kuwaonea huruma yatima. Asante kwa beti hizi nzuri.

July 18, 2009 at 9:41 AM  
Blogger Fadhy Mtanga said...

Yatima nao ni watu, huhitaji kama sisi,
Tusipungukiwe na utu, vyao tusiwafilisi,
Kwa wenye roho za kutu, hudhani hao ni nuksi.

July 26, 2009 at 10:07 AM  
Blogger Unknown said...

Good

November 27, 2019 at 2:18 AM  

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home