Friday, July 31, 2009

Dini zetu ni kikwazo.

Mola nakupa heshima,ulimwengu uliumba.
leo mimi natazama,wapo waloshayafumba.
Kisa wazi nakisema,mimi na wangu mchumba.
dini zetu ni kikwazo,e Mola tusaidie.


Sio siri nampenda,shairi nimeandika.
kwa mwingine sitoenda,mistari niliishuka.
vishawishi nitashinda,nilisema na hakika.
dini zetu ni kikwazo, e mola tusaidie.


Mapenzi hayana dini,kabila wala hayana.
semi hizi kulikoni,hatarini kuachana.
ya kweli yangu imani,kamwe siwezi ikana.
Mwenzangu yake imani,msimamo kesha weka.
dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Wazaziwe wamfunza,kiburi wamjazia.
dini yake kuitunza,msimamo wamwekea.
wazaziwe wanibeza,kifupi wanichukia.
dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Baba mama walionya,kupenda kuliniteka.
Tayari walishaona,uzoefu 'litumika.
yakwao sikuyaona,kupenda kulifunika.
Dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Mwanangu hebu tulia,wa diniyo tampata.
chunga kutokujutia,matatizo tayapata.
haya nayakumbukia,rafiki alinisuta.
dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie.


Njia panda bado nipo,sina pa kuelekea.
Nipeni njia mkato,mapenzi nayajutia.
Hima popote ulipo,ushauriwo "tapokea.

3 Comments:

Blogger Yasinta Ngonyani said...

Nitanukuu
"Mapenzi hayana dini,kabila wala hayana.
semi hizi kulikoni,hatarini kuachana.
ya kweli yangu imani,kamwe siwezi ikana.
Mwenzangu yake imani,msimamo kesha weka.
dini zetu ni kikwazo, e Mola tusaidie". Pole sana ni wengi wameshikilia hii imani ya kuolewa na kabila moja na dini moja. Hii inahuzunisha sana.

July 31, 2009 at 8:50 AM  
Blogger Fadhy Mtanga said...

Mapenzi hayana dini, nami ninasisitiza,
Dini huweza fitini, wengine kuwaumiza,
Dini wekeni pembeni, mapenzi mkayakuza,
Dini isiwe kikwazo, madhali mmependana.

Wala dini 'siwatenge, malenga nawaambia,
Mambo yenu myapange, muweze kufurahia,
Wazazi wasiwapinge, bure watawaonea,
Dini isiwe kikwazo, madhali mmependana.

Penzi halina mpaka, ati likawa na mwisho,
Usipate huzunika, mpende leo na kesho,
Awe ya kwako baraka, ni lako tunda spesho,
Dini isiwe kikwazo, madhali mmependana.

Yangu mie nimesema, usiumie moyoni,
Rafiki yangu Kissima, Mungu umtumaini,
Waeleze kwa hekima, hupendi kuf'ata dini,
Dini isiwe kikwazo, madhali mmependana.

July 31, 2009 at 9:27 PM  
Blogger Albert Kissima said...

Nashukuru kaka Fadhy,
pia nawe dada Yasinta,
ushauri wenu nimeushika.


Watoto itakuwaje,
dini gani waifuate,
hiki chasababisha, sharti pia niwaeleze.
Hima jama mnijuze,
watoto hasa itakuwaje.

July 31, 2009 at 11:51 PM  

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home