Monday, September 21, 2009

Majuto

Mtegoni nimekwama,pa kutokea sioni,
Pande zote natazama,mkombozi simuoni,
Ndugu zangu wanisema,msaada siuoni,
Siku zangu nazipima,walimwengu kwaherini.


Nahara na kutapika,mwili wote ni vidonda,
Nywele nazo zanyonyoka,natisha nilivyokonda,
Mwili wote unanuka,mauti siwezi shinda,
Saa yangu imefika,najuta niliyotenda.


Ni wengi watafuata,nakiri nilisambaza,
Wengine wameshapita,wengine wazidi cheza,
Wasomi niliwachota,fukara sikubakiza,
Kweli leo ninajuta,nsamehe Mola muweza.


Jamaa wamenitenga,ndugu waninyanyapaa,
Mawazo yananisonga,kutengwa kunaniua,
Lini kusema ntafunga,wote siku wangojea,
Maji yashazidi unga,mauti yanyemelea.


Kwa macho hutamuona,unene sio kigezo,
Vijana mliopona,hima acheni mchezo,
Gonjwa lipo kila kona,acheni vitu vya dezo,
Nakufa bado kijana,kwa Mungu mimi chukizo.

4 Comments:

Blogger Yasinta Ngonyani said...

Kissima! Huu ujumbe ni mzuri na mkali kweli nilipoanza kusoma nilianza kuogopa kidogo. Ningependa wengi wasoma ujumbe wako murwa.Ahsante .

September 21, 2009 at 12:15 PM  
Blogger Albert Kissima said...

Nafurahi kusikia hivyo dada Yasinta.

Ni kweli, nimejaribu kuweka ukali kwa kadiri iwezekanavyo, na lengo ndio hivyo, jamii iguswe na itambue kuwa gonjwa hili si masihara, na ukali uliopo ndio funzo lenyewe hasa.

September 21, 2009 at 12:42 PM  
Blogger Fadhy Mtanga said...

Majuto ni mjukuu, nawe tulishakwambia,
Hukusikia la mkuu, ukawa kiruka njia,
Umeshavunjika guu, hunapo pa kushikia,
Pole sana.

Hukusikia mwadhini, wala la mnadi sala,
Mapepe yako kichwani, maisha kuyasakala,
Walokukalisha chini, ukawaona ni mafala,
Pole sana.

Wapi walipo wenzako, niaje wamekutupa?
Leo yamefika kwako, wameanza kukukwepa,
Kwa hayo mateso yako, walahi wasingesepa,
Pole sana.

September 21, 2009 at 1:52 PM  
Blogger Albert Kissima said...

Pole yako sio kitu, mshairi nisikize,
Haisaidii katu, dunia na inifunze,
Nilikuwa mtukutu, chozi langu lipuuze.

Naisubiria saa, Mola na anichukue,
Mateso sikuzoea, fahari chanzo pekee,
Pesa nilizitumia, kwa fujo niwaambie,
Kesho zitanizikia, zilofanya niteleze.

November 9, 2010 at 7:41 AM  

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home