Monday, March 29, 2010

Nakutafuta amani.

Ajali kila uchao,maisha yanapotea,
wapo wengi hatunao,kwa mola wametangulia,
viongozi soni kwao,lawama twawatupia,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Rushwa iliyokithiri,masikini waonewa,
wakubwa wanakiburi,uchumi wahujumiwa,
pesa kitu jeuri,sheria yapinduliwa,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Ufisadi wabobea,wahusika wanafichwa,
serikali inawajua,majina wanatunziwa,
chamani waogelea,uswahiba twaelewa,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Maji ni kubwa tatizo,watu wanahangaika,
umbali sio mchezo,kina mama wanachoka,
umeme bado gumzo,ni lini taimarika,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Elimu iliyo duni,watoto wataabika,
wanakaa mavumbini,kwa shida wanaandika,
viongozi amkeni,kuonewa tumechoka,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Maisha yaliyo bora,maneno yatamkika,
walitaka hizo kura,kapuni wakatuweka,
twaishi kama chokora,na siku zinakatika,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Hii Tanzania yangu,yenye wingi wa maneno,
amani hili ni jungu,lakwaza si mfano,
amani wapi wandugu,latumika ka'ndoano,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

2 Comments:

Blogger Fadhy Mtanga said...

Amani hawi sokoni, auzwe kwa bei gani?
Afungwe kwa nailoni, nakishi atiwe ndani,
Bei yake bilioni, asimudu masikini,
Amani siyo maneno, amani huwa vitendo.

Siasa majukwaani, kutwa hubiri amani,
Kumbe mwao mioyoni, hata hawaithamini,
Wanayo ya mifukoni, mivundo yenye ubani,
Amani wanayo wao, wenye kuzitunga sera.

Amani kwa masikini, ipo tu mwake ndotoni,
Lakini si maishani, wakati hana thumuni,
Asoma magazetini, na sikio redioni,
Tamu za wanasiasa, maneno yenye kurembwa.

Sera zino vitabuni, mikakatiye pomoni,
Ila zao sizo kwani, parara zi midomoni,
Macho yeni heyoni, lila na fila zaani,
Kuhubiri wahubiri, ila matendo sifuri.

Sera za kijalalani, ama ubovu mtimani,
Hasi haiyumkini, ikatoke kundi gani,
Wote tukaibaini, ivishwe na kirauni,
Machozi yake amani, kwao hadi yakauke.

Chago chake anzuruni, urembo urujuani,
Chanzoche kili chamani, labda tuwe kijani,
Chama kile cha zamani, kichong'oa ukoloni,
Sasa siyo chetu tena, kipi kinacho amani?

Uchungu mwingi wa nini, amani kapewa nani?
Alofungia chumbani, tukose wa sebuleni,
Pengine sisi wageni, tuazime kwa jirani,
Yetu tunaifinyanga, kesho kilio kwa nani?

Kalamu naweka chini, wino upo ukingoni,
Amani usinihini, nikuweke kabatini,
Pambo wajapo wageni, wenyeji wone machoni,
Chako nje wasifia, nyumbani hakitumiki.

Kaka Albert nimelipenda sana shairi lako. Haya maoni nilokwandikia kishairi nimeona nami niyaweke kama post katika blog yangu. Utayasoma hapa http://fadhilimshairi.blogspot.com/2010/03/amani.html

Ahsante sana kwa shairi zuri.

March 29, 2010 at 2:19 PM  
Blogger Yasinta Ngonyani said...

Hakiya nani watu mna vipaji,
Ni shairi zuri, na naona mtani Fadhy amejibu kila kitu. Ahsante sana kwa tungo hizi zuri. Na mtani nawe ahsante kwa tungu hii.Upendo daima.

March 30, 2010 at 1:51 AM  

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home