Friday, October 9, 2009

Maisha

Maisha kweli ni fumbo,lilogumu kufumbua,
Leo lakupiga kumbo,kesho wachekelea,
Punde yezaenda kombo,sharti kujikwamua,
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.


Maisha yamesheheni,uzuri pia ubaya,
Ungalipo duniani,usiyaonee haya,
Popote yatafuteni,msichoke kusakanya,
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.


Usitukane wakunga,na uzazi bado upo,
Mlango utafunga,ungali ndani haupo,
Meli maisha tasonga,taachwa hapo ulipo.
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.


Njiani utayakuta,majabali vizingiti,
Huna budi kuyapita,viunzi havikwepeki,
Kamwe hakuna kujuta,maisha nasbu bahati,
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.

2 Comments:

Blogger Fadhy Mtanga said...

Maisha pia safari, yataka uvumilivu,
Vema kuyatafakari, na tena kwa uzamivu,
Maisha siyo kamari, hayahitaji ubavu.

Maisha ni fumbo kweli, tulia kulifumbua,
Ufikiri mara mbili, siyo kukurupukia,
Upate ilo halali, haramu kuikimbia.

Maisha ndiyo maisha, enenda mwendo salama,
Usijaribu jitwisha, mzigo wenye kuuma,
Leo ninakukumbusha, na Kissima keshasema.

October 9, 2009 at 8:51 AM  
Blogger Yasinta Ngonyani said...

Maisha ni safari ndefu,
Yahitaji uangalifu
Mungu ndiye ajuaaye siku moja atatujalia mema.

October 10, 2009 at 11:15 AM  

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home