Friday, May 20, 2011

Ajali zaepukika!

Jamani nisikizeni, nisomeni waungwana,
Nafichani moyoni, lipi lisojulikana,
Ajali tele pomoni, usiku hata mchana,
Madereva mwahusika, ajali zaepukika.

Wa mabasi wamiliki, amueni mtaweza,
Andaeni mikakati, ajali kutokomeza,
Magari muyahakiki, kabla safari kuanza.
Madereva yao haki, wapeni bila kupinda.

Ulevi na muuache, madereva mwahusika.
Subiri hima kukuche, usiku hamtafika.
Sheria mzitumie, mnazitambua fika.
Madereva mtulie, ajali zaepukika.

Ajali zimekithiri, za mabasi si kificho,
Vita si ya hiari, fungueni yenu macho,
Maisha ya wasafiri, bora ya mboni ya jicho,
Kukumbushwa msisubiri, ajali zaepukika.

Abiria kataeni, mwendo uliomkali,
Roho zenu teteeni, si budi kuwa wakali,
Mikanda katika siti, fungeni kwa kila hali.
Wasafiri unganeni, uhai wenu chungeni.

Polisi barabarani, mwahusika siwafichi,
Rushwa sasa acheni, wateteeni wananchi,
Magari ya'lo walakini, hakikisha huyaachi.
Usalama dumisheni, ajali 'taepukika.

Wasanii Five Star, walipoteza maisha,
Ajali twakumbukia, uzembe lisababisha,
Mv bukoba nakumbushia, uzembe umetutosha,
Meli ilielemea, ukweli sitopindisha.

Amani umetutoka, Kessy tulikuhitaji,
Tunalia tunachoka, ajali "mekuwa jaji,
Ajalini 'mekufika, mauti yasotaraji,
Ajali 'metunyang'anya, rafiki yetu mkubwa.

Abiria ushikeni, huu wangu ushauri,
Kulala na epukeni, pindi mnapo safiri,
Magazetini kunani, iwe mwisho wa safari.
Hakuna jipya fanani, yote nayakariri.

Sina tena la ziada, zinaepukika ajali,
Hebu hii iwe mada, namna ya kukabili,
Uhai vema kulinda, tena kwa hali na mali.
Janga si la kawaida, tujipange kukabili.

7 Comments:

Blogger Fadhy Mtanga said...

ahsante sana kaka kwa shairi maridhawa hili. Ulipotea sana, lakini ni furaha iliyoje kusoma tena tungo zako.

May 22, 2011 at 3:01 AM  
Blogger Albert Kissima said...

Nashukuru kaka Fadhy, nipo tena kundini.

May 22, 2011 at 3:39 AM  
Blogger wilbert mukasa said...

hongera kaka,amani alikuwa rafiki yetu kipenzi,mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.amen

May 22, 2011 at 5:33 AM  
Blogger Albert Kissima said...

Ni majonzi, ni huzuni kaka Wilbert. Tumeondokewa na Rafiki na ndugu yetu Amani Kessy, ambaye bado tulimuhitaji. Mungu kampenda zaidi. Mungu alitoa, Mungu ametwaa; jina lake lihimidiwe. Mola ailaze Roho ya marehemu mahala pema peponi; Amen.

May 22, 2011 at 9:34 AM  
Blogger Yasinta Ngonyani said...

Hakika wakati mwingine huwa najiuliza sijui kweli hawa madereva walipata hizi linces kiukweli au...ila kweli ugimbi ndio unaosaidia hizi ajali pia haya mapulizo...Pole kaka Albert kwa kumpoteza rafiki kwani rafiki yako ni rafiki yangu..Apumzike kwa amani.

May 24, 2011 at 1:27 PM  
Anonymous jigambeads said...

This blog very interesting but you can also try these ..www.jigambeads.com and ..www.tanzaniakwetu.com for popularity and more advert to advertise. Thanks

December 2, 2011 at 6:35 AM  
Anonymous Profee said...

Nimependa sana fonts, contents arrangement ya hii blog bt tupe wadau wako Updates zaidi ila picture hakuna ndugu.
Ukiweza pitia
www.TanzaniaKwetu.com
na if possible jaribu kuisajili blog yako kule jus kuongeza viewers.

Tupo pamoja Mtanzania!

December 5, 2011 at 12:35 AM  

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home