Tuesday, February 14, 2012

Nyota

Waridi nakutafuta, shairi niliandika,
Siku nazo zikapita, mwandani nilimsaka,
Sasa nimeshampata, wakati umeshafika,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Nyota unanisikia, ninakupenda kwa dhati,
Thamaniyo naijua, ya dhahabu haikuti,
Kuwa nawe najivunia, daima wala sijuti,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Ukitaka nitafune, ukitaka unimeze,
Utamuwo wa senene, Wahaya na waeleze,
Si mwembamba si mnene, wa wastani nikujuze,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Asante kwa kunijali, thamani kubwa wanipa,
Hujanipenda kwa mali, mapungufu hujakwepa,
Tupitazo zote hali, hutanitenga 'meapa,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Washibisha nafsi yangu, Nyota nakuambia,
Waujaza moyo wangu, kwa penzi 'lilotimia,
Heko malaika wangu, kwa penzi li'lotulia,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Nyota ninamaanisha, Stella maana yake,
Urembo usiokwisha, hii sifa yake,
Nakupenda wa maisha, ujumbe hima ufike,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.