Monday, September 21, 2009

Majuto

Mtegoni nimekwama,pa kutokea sioni,
Pande zote natazama,mkombozi simuoni,
Ndugu zangu wanisema,msaada siuoni,
Siku zangu nazipima,walimwengu kwaherini.


Nahara na kutapika,mwili wote ni vidonda,
Nywele nazo zanyonyoka,natisha nilivyokonda,
Mwili wote unanuka,mauti siwezi shinda,
Saa yangu imefika,najuta niliyotenda.


Ni wengi watafuata,nakiri nilisambaza,
Wengine wameshapita,wengine wazidi cheza,
Wasomi niliwachota,fukara sikubakiza,
Kweli leo ninajuta,nsamehe Mola muweza.


Jamaa wamenitenga,ndugu waninyanyapaa,
Mawazo yananisonga,kutengwa kunaniua,
Lini kusema ntafunga,wote siku wangojea,
Maji yashazidi unga,mauti yanyemelea.


Kwa macho hutamuona,unene sio kigezo,
Vijana mliopona,hima acheni mchezo,
Gonjwa lipo kila kona,acheni vitu vya dezo,
Nakufa bado kijana,kwa Mungu mimi chukizo.

Friday, September 11, 2009

Jua ni la utosini.

Asubuhi kunakucha,na njia ninaishika,
Ninapokwenda naficha,'tasema ntakapofika,
Nitapata ya mchicha?,swali liso na hakika,
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Ni wangu tena ujio,fungua pesa upate,
Chanuo na mafagio,ina njoo nikupake,
Anjifu na mitandio,mikufu pia na pete,
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Huruma siku yapita, ndururu sijainusa,
Watoto mimi najuta,viumbe waso na kosa,
Mitaa ninaipita,wateja spati kabisa,
Jua linanifuata,katu halitaki susa,
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Machinga ndo kazi yangu,mtaa hadi mtaa,
Kazi yanipa machungu,ila sikati tamaa,
Nachoka haki ya Mungu,umande nilikimbia.
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Mlo bahati someni, mwenzenu nilichezea,
Chenga nyingi shuleni,vitabu sikushangaa,
wasomi mataikuni,tuso skuli twaduwaa.
Jua ni la utosini,linachoma si utani.


Siombee umachinga,miguu yote yauma,
Bora jela kutinga,jua la utosi noma,
Pesa haujaichanga,fasta jua lishazama.
Jua ni la utosini,linachoma si utani.

Saturday, September 5, 2009

Wosia wa Babu

Wajukuu sikizeni,muda wangu umekwisha.
Leo nimewaiteni, muhimu kuwasilisha.
Sikiliza kwa makini,wala sitaki wachosha.


Mkamateni elimu,msimwache aendeze.
Hii ni nguzo muhimu,ili maisha uweze.
Hili ni langu jukumu,nawasihi muutunze.

Cha mwenzako si cha kwako,hilo sharti mlijue.
Tumia akili yako,muulize kapataje.
Kuiba na iwe mwiko,kwa jasho jitafutie.


Kweli kuweni makini,gonjwa lipo mtaani.
vya dezo kataeni,misaada tambueni.
'Siishi kwa tumaini,hasara tele nyumbani.

Maisha si lelemama,juhudi inawapasa.
Msikubali kukwama,sekunde hata lisaa.
Pande zote na tazama,pa kuanza hutokosa.

Kueni wavumilivu,matatizo yakabili.
Katu msiwe wavivu,msibaki na kandili.
Msile ulo mkavu,tulia penye kivuli.

Nguvu zinaniishia,nilosema yashikeni,
Huu ndo wangu wosia,ushikeni akilini.
Dunia itawambia,pembueni kwa makini.