Tuesday, February 14, 2012

Nyota

Waridi nakutafuta, shairi niliandika,
Siku nazo zikapita, mwandani nilimsaka,
Sasa nimeshampata, wakati umeshafika,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Nyota unanisikia, ninakupenda kwa dhati,
Thamaniyo naijua, ya dhahabu haikuti,
Kuwa nawe najivunia, daima wala sijuti,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Ukitaka nitafune, ukitaka unimeze,
Utamuwo wa senene, Wahaya na waeleze,
Si mwembamba si mnene, wa wastani nikujuze,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Asante kwa kunijali, thamani kubwa wanipa,
Hujanipenda kwa mali, mapungufu hujakwepa,
Tupitazo zote hali, hutanitenga 'meapa,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Washibisha nafsi yangu, Nyota nakuambia,
Waujaza moyo wangu, kwa penzi 'lilotimia,
Heko malaika wangu, kwa penzi li'lotulia,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Nyota ninamaanisha, Stella maana yake,
Urembo usiokwisha, hii sifa yake,
Nakupenda wa maisha, ujumbe hima ufike,
Nyota wangu unang'aa, daima nitakupenda.

Friday, December 23, 2011

Laiti angekuwepo

Kauli i'lozagaa, ya tamaa kuikata,
U wapi u'lotufaa, twatamani kukufwata,
Nchi inachechemea, ni mengi yanatukuta,
Laiti angekuwepo, mbona Kingunge tunaye?

Ngombale bado tunaye, hima tumtumieni,
Nyerere hatupo naye, fikra'ze zipo vichwani,
Busara'ze ajuaye, Kingunge hoja mezani.
Laiti angekuwepo, Mama Nyerere tunaye.

Mama yetu wa Taifa, ana mengi kutufunza,
Laiti hii ni kashfa, mama bado anaweza,
Kujuta wala si sifa, busara'ze si kubeza,
Laiti angekuwepo, Malecela mbona yupo?

Tokea enzi za baba, alikuwapo Msuya,
Busara alizishiba, wala takrima hakula,
Mbinu bado kazibeba, atumiwe bila hila,
Laiti angekuwepo, mbona wengi bado wapo?

Hebu tuwape nafasi, historia wapakue,
Makovu yake nanasi, utamu'we palepale,
Tuache mawazo hasi, wazee wasaidie,
Laiti angekuwepo, wapo tuwatumieni.

Laiti si neno zuri, twende mbele Tanzania,
Uzalendo ndio siri, tujibidishe kwa nia,
Bila Nyerere si shwari, msemo wa mazoea,
Laiti angekuwepo, mawazoye twatumia?

Wapo wengi wa zamani, enzi zile za Mwalimu,
Ni wachache shairini, wote kuwepo ni ngumu,
Tupeni dira jamani, wa mwalimu mu muhimu,
Laiti angekuwepo, Mpo wengi m'lo tunu.

Friday, May 20, 2011

Ajali zaepukika!

Jamani nisikizeni, nisomeni waungwana,
Nafichani moyoni, lipi lisojulikana,
Ajali tele pomoni, usiku hata mchana,
Madereva mwahusika, ajali zaepukika.

Wa mabasi wamiliki, amueni mtaweza,
Andaeni mikakati, ajali kutokomeza,
Magari muyahakiki, kabla safari kuanza.
Madereva yao haki, wapeni bila kupinda.

Ulevi na muuache, madereva mwahusika.
Subiri hima kukuche, usiku hamtafika.
Sheria mzitumie, mnazitambua fika.
Madereva mtulie, ajali zaepukika.

Ajali zimekithiri, za mabasi si kificho,
Vita si ya hiari, fungueni yenu macho,
Maisha ya wasafiri, bora ya mboni ya jicho,
Kukumbushwa msisubiri, ajali zaepukika.

Abiria kataeni, mwendo uliomkali,
Roho zenu teteeni, si budi kuwa wakali,
Mikanda katika siti, fungeni kwa kila hali.
Wasafiri unganeni, uhai wenu chungeni.

Polisi barabarani, mwahusika siwafichi,
Rushwa sasa acheni, wateteeni wananchi,
Magari ya'lo walakini, hakikisha huyaachi.
Usalama dumisheni, ajali 'taepukika.

Wasanii Five Star, walipoteza maisha,
Ajali twakumbukia, uzembe lisababisha,
Mv bukoba nakumbushia, uzembe umetutosha,
Meli ilielemea, ukweli sitopindisha.

Amani umetutoka, Kessy tulikuhitaji,
Tunalia tunachoka, ajali "mekuwa jaji,
Ajalini 'mekufika, mauti yasotaraji,
Ajali 'metunyang'anya, rafiki yetu mkubwa.

Abiria ushikeni, huu wangu ushauri,
Kulala na epukeni, pindi mnapo safiri,
Magazetini kunani, iwe mwisho wa safari.
Hakuna jipya fanani, yote nayakariri.

Sina tena la ziada, zinaepukika ajali,
Hebu hii iwe mada, namna ya kukabili,
Uhai vema kulinda, tena kwa hali na mali.
Janga si la kawaida, tujipange kukabili.

Monday, October 4, 2010

Joka mbona huzeeki?

Upo toka Tanganyika, hadi sasa Tanzania,
Msingi aliuweka, baba kesha tangulia,
Tayari tungeshafika, Nyerere angendelea,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Chumvi yote ulokula, tumia basi busara,
Ifike tena pahala, hima iamue kura,
Watu ndio wenye hila, chombo hakina papara,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Wajengao hicho chombo, kizalendo watafteni,
Ndani kimejaa shombo, chaoshwa kwenye kampeni,
Waambulia kikumbo, watetezi wa maskini,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Kalamu ninaiacha,wino kamwe hutokwisha,
Joka ondoa makucha, malengo kufanikisha,
Tazama panavyokucha, huna budi kutupisha,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Uzee busara bwana, zeeka inakubidi,
Kwanini unang'ang'ana , twajua ushafaidi,
Wapeni nao vijana, tuifikie ahadi,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Monday, March 29, 2010

Nakutafuta amani.

Ajali kila uchao,maisha yanapotea,
wapo wengi hatunao,kwa mola wametangulia,
viongozi soni kwao,lawama twawatupia,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Rushwa iliyokithiri,masikini waonewa,
wakubwa wanakiburi,uchumi wahujumiwa,
pesa kitu jeuri,sheria yapinduliwa,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Ufisadi wabobea,wahusika wanafichwa,
serikali inawajua,majina wanatunziwa,
chamani waogelea,uswahiba twaelewa,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Maji ni kubwa tatizo,watu wanahangaika,
umbali sio mchezo,kina mama wanachoka,
umeme bado gumzo,ni lini taimarika,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Elimu iliyo duni,watoto wataabika,
wanakaa mavumbini,kwa shida wanaandika,
viongozi amkeni,kuonewa tumechoka,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Maisha yaliyo bora,maneno yatamkika,
walitaka hizo kura,kapuni wakatuweka,
twaishi kama chokora,na siku zinakatika,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Hii Tanzania yangu,yenye wingi wa maneno,
amani hili ni jungu,lakwaza si mfano,
amani wapi wandugu,latumika ka'ndoano,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Sunday, December 20, 2009

Waridi.

Ua ninakutafuta, tayari ushachanua,
Marashi nanayapata,manukato yavutia,
Ni lini nitakupata,uzuri najivunia,
Waridi nakutafuta, nataka kujichumia.


Niite unionapo, wala usibabaike,
Sijui wapi ulipo,paza sauti iskike,
Ipi ni njia mkato, haraka mimi nifike,
Waridi nakutafuta, nataka kujichumia.


Ni mengi ninayaona, maua ya kupendeza,
Ni lipi lililonona,si kazi ya kubeza,
Waridi ndo lanikuna,ua litaniliwaza,
Waridi nakutafuta, nataka kujichumia.

Waridi ninakusaka,wa maisha jitokeze,
Mbali pia nitafika,ulipo wewe nijuze,
ua umeshapevuka,nakuchuma nikutunze,
Waridi nakutafuta, nataka kujichumia.

Bustanini ninapita,tayari kujichumia,
Tabia itanivuta,ua kufuatilia,
Najua nitalipata,maisha tafurahia.
Waridi nakutafuta, nataka kujichumia.

Friday, October 9, 2009

Maisha

Maisha kweli ni fumbo,lilogumu kufumbua,
Leo lakupiga kumbo,kesho wachekelea,
Punde yezaenda kombo,sharti kujikwamua,
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.


Maisha yamesheheni,uzuri pia ubaya,
Ungalipo duniani,usiyaonee haya,
Popote yatafuteni,msichoke kusakanya,
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.


Usitukane wakunga,na uzazi bado upo,
Mlango utafunga,ungali ndani haupo,
Meli maisha tasonga,taachwa hapo ulipo.
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.


Njiani utayakuta,majabali vizingiti,
Huna budi kuyapita,viunzi havikwepeki,
Kamwe hakuna kujuta,maisha nasbu bahati,
Maisha ndivyo yalivyo,ya kesho huwezi jua.