Monday, October 4, 2010

Joka mbona huzeeki?

Upo toka Tanganyika, hadi sasa Tanzania,
Msingi aliuweka, baba kesha tangulia,
Tayari tungeshafika, Nyerere angendelea,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Chumvi yote ulokula, tumia basi busara,
Ifike tena pahala, hima iamue kura,
Watu ndio wenye hila, chombo hakina papara,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Wajengao hicho chombo, kizalendo watafteni,
Ndani kimejaa shombo, chaoshwa kwenye kampeni,
Waambulia kikumbo, watetezi wa maskini,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Kalamu ninaiacha,wino kamwe hutokwisha,
Joka ondoa makucha, malengo kufanikisha,
Tazama panavyokucha, huna budi kutupisha,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Uzee busara bwana, zeeka inakubidi,
Kwanini unang'ang'ana , twajua ushafaidi,
Wapeni nao vijana, tuifikie ahadi,
Joka mbona huzeeki, binafsi nimekuchoka.

Monday, March 29, 2010

Nakutafuta amani.

Ajali kila uchao,maisha yanapotea,
wapo wengi hatunao,kwa mola wametangulia,
viongozi soni kwao,lawama twawatupia,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Rushwa iliyokithiri,masikini waonewa,
wakubwa wanakiburi,uchumi wahujumiwa,
pesa kitu jeuri,sheria yapinduliwa,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Ufisadi wabobea,wahusika wanafichwa,
serikali inawajua,majina wanatunziwa,
chamani waogelea,uswahiba twaelewa,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Maji ni kubwa tatizo,watu wanahangaika,
umbali sio mchezo,kina mama wanachoka,
umeme bado gumzo,ni lini taimarika,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Elimu iliyo duni,watoto wataabika,
wanakaa mavumbini,kwa shida wanaandika,
viongozi amkeni,kuonewa tumechoka,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Maisha yaliyo bora,maneno yatamkika,
walitaka hizo kura,kapuni wakatuweka,
twaishi kama chokora,na siku zinakatika,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.

Hii Tanzania yangu,yenye wingi wa maneno,
amani hili ni jungu,lakwaza si mfano,
amani wapi wandugu,latumika ka'ndoano,
Nakutafuta amani,waongewa sikuoni.